Utaratibu maalum wa mikopo unawapa wakulima wenye uzoefu, wakiwemo vijana wa mpango waBuilding a Better Tomorrow (BBT), fursa ya kupiga hatua kuelekea kilimo cha kibiashara kwa kiwango kikubwa, kupitia teknolojia ya umwagiliaji inayotumia nishati ya jua, yenye hati miliki nchini Marekani, na inayopunguza utegemezi wa mvua za msimu.
DAR ES SALAAM, TANZANIA – Dronlytics Technologies Tanzania Limited na Azania Bank Plc leo wametangaza utaratibu maalum wa mikopo ya kilimo kwa wakulima wadogo, wakiwemo vijana wakulima, wanaoshiriki katika Programu ya Dronlytics Block Farm mkoani Morogoro. Utaratibu huu unaendeleza ushirikiano wa kimkakati ulioidhinishwa rasmi mapema mwaka huu kwa kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU), na unajenga juu ya mpango wa Serikali wa Building a Better Tomorrow: Youth Initiative for Agribusiness (BBT-YIA), kwa kuwapa vijana waliopata uzoefu wa vitendo katika kilimo njia ya kufikia kilimo cha kibiashara kwa kiwango kikubwa. Vijana wakulima wa kwanza wanatarajiwa kujiunga na programu katika robo ya kwanza ya mwaka 2027.
Ushirikiano huu unaunganisha uwezo wa Azania Bank katika kutoa mikopo ya kilimo na mbinu jumuishi ya Dronlytics ya kufanya kilimo cha wakulima wadogo kuwa cha kisasa, kwa kutegemea mfumo wa umwagiliaji wenye hati miliki nchini Marekani ambao Dronlytics inauleta Tanzania.
Kuendeleza Mafanikio ya Programu ya BBT
Programu ya BBT-YIA ya Wizara ya Kilimo huwapatia vijana wa Tanzania mafunzo na nafasi za kushiriki katika biashara ya kilimo kama sehemu ya Ajenda ya Taifa ya 10/30. Programu ya Dronlytics Block Farm imeundwa kuwa hatua inayofuata kwa vijana wa BBT na vijana wengine wakulima wenye uzoefu wa kilimo wa angalau miezi 12, ambao wako tayari kupanua shughuli zao zaidi ya mashamba yao ya awali. Programu hii imepokea idhini ya kuungwa mkono kama mradi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa kuwa programu hii inaunganisha shughuli zote kuanzia mbegu hadi soko la mwisho, matumizi jumuishi ya mitambo ya kilimo na huduma za kilimo zinazosimamiwa kwa pamoja huwawezesha wakulima wanaoshiriki kuendesha mashamba makubwa zaidi, huku wakitumia muda wao zaidi katika usimamizi na uendelezaji wa biashara.
Teknolojia ya Umwagiliaji Yenye Hati Miliki: Kutoka Mavuno Moja kwa Mwaka hadi Matatu
Kiini cha programu hii ni mfumo wa umwagiliaji uliothibitishwa na wenye hati miliki nchini Marekani, unaowezesha kuongeza mavuno kutoka mzunguko mmoja wa kilimo unaotegemea mvua kwa mwaka hadi mizunguko mitatu. Kwa kuyafikisha maji kwa usahihi mahali na wakati mazao yanapoyahitaji, mfumo huu unaotumia nishati ya jua unaondoa utegemezi wa uzalishaji kwa mvua za msimu na kuwezesha mzunguko wa kilimo cha mpunga na soya mwaka mzima.
Mfumo huu tayari unatumika kibiashara katika mashamba nchini Marekani. Unajumuisha teknolojia ya kukusanya na kurejesha maji yanayotiririka kutoka shambani (tailwater recovery), yenye hati miliki ya Chuo Kikuu cha Arkansas, ambayo hukusanya na kutumia tena maji na pembejeo ndani ya shamba, hivyo kuzuia mtiririko wake kwenda kwenye vijito na mito ya jirani. Matokeo yake yanathibitishwa na utafiti huru: utafiti wa miaka mitatu uliofanywa na Kituo cha Utafiti na Ugani wa Mpunga cha Chuo Kikuu cha Arkansas ulibaini kuwa mfumo huo ulipunguza matumizi ya maji kwa wastani wa asilimia 67 na matumizi ya mbolea kwa asilimia 30, bila athari kubwa kwa mavuno. Mashamba yanayomwagiliwa kwa usahihi na yasiyofunikwa na maji muda wote pia hutoa gesi ya methane kidogo kuliko mashamba ya mpunga yanayokuwa na maji yaliyotuama wakati wote.
Badala ya kumiliki na kusimamia teknolojia hii peke yake, Dronlytics inaiwezesha kupatikana moja kwa moja kwa wakulima wa Tanzania, ambao hununua na kumiliki mifumo yao ya umwagiliaji kupitia mikopo ya Azania Bank na dhamana ya muda mrefu ya bidhaa (warranty) inayotolewa na Dronlytics. Mfumo huu unakamilishwa na ufuatiliaji wa mashamba kwa kutumia ndege zisizo na rubani (droni), pamoja na jukwaa la teknolojia la Dronlytics linalounganisha taarifa za shambani na za satelaiti ili kufuatilia hali ya mazao, udongo na maji. Hivyo, kilimo cha usahihi kinakuwa rahisi kufikiwa na wakulima wadogo.
Jinsi Programu ya Block Farm Inavyofanya Kazi
Programu hii inawapa vijana wakulima fursa ya kufanya kilimo chenye tija kwa kiwango kikubwa kwa kutumia miundombinu, huduma na masoko ambayo mara nyingi hayapatikani kwa urahisi kwa mkulima mdogo mmoja mmoja. Wakulima hukodisha ardhi kutoka Dronlytics kwa makubaliano ya muda mrefu, wakianza na ekari 4, 6 au 10, huku wakiwa na fursa ya kupanua mashamba yao kadri Dronlytics inavyokua. Umwagiliaji wa mwaka mzima huwawezesha wakulima kufuata mzunguko uliopangwa wa mpunga–soya–mpunga, na kupata hadi mavuno matatu kwa mwaka. Dronlytics hununua mazao yote mawili wakati wa mavuno.
Lengo la Dronlytics ni kuwawezesha wakulima kupata kipato halisi kinachofikia takriban mara tano ya kipato kinachopatikana katika mfumo unaolinganishwa nao wa kilimo cha mpunga cha msimu mmoja unaotegemea mvua. Hii itawapa wakulima wadogo njia ya kuongeza kipato, kujenga mali na kuimarisha usalama wao wa kifedha. Mzunguko wa kilimo cha soya pia unaunga mkono kipaumbele cha taifa katika kilimo, unaboresha afya ya udongo na kusaidia kukatiza mizunguko ya wadudu waharibifu na magonjwa.
“Tunabadilisha maana ya kilimo kwa vijana wa Tanzania. Kwa kuweka teknolojia mikononi mwao na kuwawezesha kupata hadi mavuno matatu kwa mwaka, tunabadilisha kilimo kutoka kuwa chaguo la mwisho na kukifanya kuwa biashara yenye mustakabali unaofaa kuwekeza nguvu na rasilimali. Tunapofikia lengo letu la ekari 50,000, tuna uwezo wa kuwawezesha hadi vijana wakulima 12,500, kunufaisha takriban watu 50,000 katika kaya zao, na kuchochea ajira nyingi zaidi katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo. Tunataka vijana wa Tanzania wachague kilimo kwa hiari, badala ya kukifanya kwa kukosa fursa nyingine.” — Anthony Hall, Afisa Mtendaji Mkuu, Dronlytics Technologies Tanzania Limited
Kuunganisha Wakulima na Masoko
Programu hii inaungwa mkono pia na mkataba wa ununuzi wa mazao (offtake agreement) na Wilmar Rice Tanzania Limited, sehemu ya Wilmar International, kampuni iliyomo katika orodha ya Fortune Global 500. Mkataba huu unaunganisha moja kwa moja uzalishaji wa mashamba uliopangwa na mnyororo wa thamani wa mpunga nchini Tanzania.
“Upatikanaji wa mpunga bora, kwa uhakika na kwa kiwango kinachoweza kuongezeka, ni muhimu kwa sekta ya mpunga nchini Tanzania. Mfumo wa Dronlytics wa uzalishaji uliopangwa na ushiriki wa wakulima unaoratibiwa kwa utaratibu maalum unatupa imani katika uthabiti wa upatikanaji na ubora wa mpunga tunaopokea, hasa kadri programu inavyopanuka.” — Bw. Vinod Kumar, Meneja Mkuu, Wilmar Rice
Ushirikiano Ulioundwa kwa Ajili ya Upanuzi
Dronlytics inalenga kuendeleza ekari 50,000 ndani ya miaka mitano. Kila shamba jipya katika Programu ya Block Farm litawawezesha wakulima wanaokidhi vigezo kupanua shughuli zao, huku likitoa fursa kwa vijana wakulima wengine kujiunga na programu. Mikopo inayotolewa na Azania Bank inaweka msingi wa upanuzi huu na uwezeshaji wa kiuchumi wa vijana wakulima wadogo wa Tanzania.
“Tunaiona Programu ya Dronlytics Block Farm kuwa mfano mzuri wa jinsi mikopo ya kilimo inavyoweza kusaidia uwezeshaji na mageuzi kwa vijana wakulima, kwa kuwaunganisha na rasilimali za uzalishaji, kilimo kinachoratibiwa na upatikanaji wa masoko. Utaratibu huu maalum wa mikopo unaakisi dhamira yetu ya kusaidia kilimo chenye uwezo wa kufanikiwa kibiashara, huku tukishiriki katika mfumo ulioundwa ili kuwezesha upanuzi na usimamizi bora wa mikopo ya kilimo kwa wakulima wadogo.” — Bw. Augustino Matutu, Mkuu wa Kitengo cha Biashara ya Kilimo, Azania Bank Plc
Ushirikiano kati ya Dronlytics na Azania Bank unaendeleza malengo ya mpango wa Serikali wa BBT-YIA, kwa kufanya kilimo chenye tija kuwa njia ya kuongeza kipato cha kaya, kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ajira vijijini na kupanua ujumuishi wa kifedha, huku ukilinda ardhi, maji na mazingira asilia ya Tanzania.







